Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema mazungumzo ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kati ya CCM na ACT-Wazalendo yanaendelea vizuri huku CCM ikiwa tayari kushiriki katika kuunda Serikali hiyo kwa maslahi ya Taifa na wananchi.
Dkt. Mwinyi amesema hayo leo tarehe 09 Mei 2026 alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja katika mkutano wa kutoa shukrani baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Katika Ukumbi wa Afisi za CCM Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja
Amesema CCM itaendelea kusimamia kwa umakini na busara mchakato huo huku ikilinda maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla. Aidha, amewataka viongozi na wanachama wa CCM kufanya tathmini baada ya uchaguzi na kujipanga mapema kwa Uchaguzi wa mwaka 2030 pamoja na uchaguzi wa ndani ya Chama.
Halikadhalika, Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, maadili ya uongozi, utekelezaji wa Ilani, kuimarisha uchumi wa Chama na Taifa pamoja na kulinda amani nchini. Pia amesema Serikali inaendelea kuimarisha uchumi wa Zanzibar kupitia maboresho ya miundombinu ya bandari na juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia vyanzo mbadala ikiwemo jua, upepo na gesi asilia.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Mwinyi amewahimiza viongozi na wanachama wa CCM kuendelea kushikamana na kukiimarisha Chama katika ngazi zote.
