Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu na jamii kwa ujumla kuendeleza utaratibu mzuri wa kuwasaidia na kuwahurumia watu wasio na uwezo kwa kuzingatia mahitaji yao maalumu. Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 21 Machi 2026, katika Baraza la Eid el-Fitri lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Polisi, Ziwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amefafanua kuwa ili kuwa na jamii yenye ustawi bora, ni vema utaratibu huo ukaendelezwa kwani kwa kiasi kikubwa umewasaidia watu wa makundi maalumu, wakiwemo mayatima, wajane na mafakiri, kupata futari na kutekeleza ibada ya funga kikamilifu. Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema waumini wa dini ya Kiislamu wana wajibu mkubwa wa kutekeleza na kuendeleza mambo yote ya kheri yaliyokuwa yakifanyika katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ikiwemo kumcha Mwenyezi Mungu kwa bidii, kwani yanaongeza upendo, umoja na mshikamano.

Akizungumzia Sikukuu ya Eid el-Fitri, amelitaka Jeshi la Polisi kusimamia na kuhakikisha usalama na amani vinaimarishwa katika viwanja vya sikukuu, pamoja na kusisitiza usimamizi madhubuti wa sheria za usalama barabarani ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu kwa amani na utulivu.

Kwa upande wa suala la Hijjah, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zinazosafirisha mahujaji kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana ili kuhakikisha Waislamu wanaokwenda kutekeleza ibada ya Hijjah wanaongezeka. Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utaratibu wa kukamilisha kuanzishwa kwa mfuko maalum wa Hijjah.

Baraza la Eid limehudhuriwa na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi, viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein, Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu, Balozi Seif Ali Iddi, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zuberi Ali Maulid, pamoja na viongozi wa dini, masheikh na waumini mbalimbali.