WAZIRI wa Kazi,Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Moudline Castico ameipongeza jamii ya Wazanzibar kwa juhudi inazozichukuwa katika utunzaji wa familia, na hivyo kupunguza tatizo la utupaji wa watoto ovyo.
Ametowa pongezi hizo kituo cha kulelea watoto Mazizini, wakati akitowa neno la shukrani baada ya hafla ya Futari iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Suleiman Idd, kwa ajili ya watoto wa kituo hicho.
Alisema ni jambo la faraja kuona katika siku za hivi karibuni vitendo ya utupaji wa watoto vimepungua, hatua aliyobainisha inatokana na juhudi za wananchi katika utunzaji wa familia zao.
Aliiomba jamii kuendelea na juhudi hizo zinazotokana na ushirikiano wa pamoja kati ya jamii hiyo na Serikali.
Aidha, Waziri Castico alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi hao kutokana na mchango mkubwa wanaouonyeha katika kuleta maendeleo na ustawi bora wa watoto hapa nchini, ikiwemo wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Alisema hafla hiyo iliyowahusisha watoto wanaolelewa katika kijiji hicho inadhihirisha imani na mapenzi makubwa waliyonayo viongozi hao kwa watoto hao, hivyo akawaomba kuendelea kuwa karibu nao katika vipindi vyote.
Katika hatua nyengine, Waziri Castico aliutaka uongozi wa kituo hicho kuendelea kuwatunza vyema watoto hao, sambamba na kutoa indhari ya kuwepo umakini wa kiusalama katika kipindi cha sherehe ya sikukuu ya Idd el Fitri.