Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Zanzibar inahitaji kuwa na vyuo vikuu zaidi vitakavyosaidia kuiweka Zanzibar katika ramani ya kimataifa kama kituo muhimu cha utoaji wa mafunzo na elimu ya viwango vya juu katika fani mbalimbali.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 18 Februari 2026, alipokutana na wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mhe. Mussa Azan Zungu, waliofika Ikulu, Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameridhishwa na wazo la Bunge la ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Diplomasia na Huduma za Bunge kinachotarajiwa kujengwa Zanzibar, akieleza kuwa mradi huo ni fursa adhimu kwa taifa. Amesema kuwa uwepo wa chuo hicho utachochea ujio wa wanafunzi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali kuja kujifunza Zanzibar, hali itakayochangia kukuza uchumi na kuongeza mapato ya nchi kupitia sekta ya elimu na huduma zinazohusiana nayo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wajumbe hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo, na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo kulifanikisha wazo hilo kwa haraka ili Zanzibar iweze kunufaika na fursa hiyo mapema.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake thabiti ulioleta mabadiliko makubwa ya maendeleo Zanzibar, hususan katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na kasi ya ukuaji wa uchumi inayoendana na mabadiliko ya dunia.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge wako Zanzibar kwa ajili ya mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa Kamati ya Uongozi na Tume ya Utumishi ya Bunge, yaliyofanyika Tunguu, Mkoa wa Kusini, Unguja.