RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa mashirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania ili Ofisi hiyo iweze kutekeleza vyema majukumu yake katika kuimarisha demokrasia nchini Dk. Shein aliyasema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Mohammed Ali Ahmed aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais akiwa amefuatana na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi.
Katika maelezo yake Rais Dk. alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa Ofisi hiyo pamoja na uongozi wake kwa Taifa, hivyo kuna kila sababu ya kutoa ushirikiano wake kwa lengo la kuimarisha demokrasia.Dk. Shein alimpongeza Naibu Msajili huyo wa Vyama vya siasa kwa kuteuliwa nafasi hiyo na kueleza matumaini yake makubwa ya utendaji kazi wa kiongozi huyo.
Aidha, Rais Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kwamba kwa upande wa Zanzibar atapewa kila aina ya msaada na mashirikiano ili aweze kufanikisha kazi zake vyema hasa ikizingatiwa kuwa ofisi yake ipo hapa Zanzibar.
Nae Jaji Francis Mutungi aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa mashirikiano makubwa inayoyapata Ofisi yake hatua ambayo imeweza kusaidia kufanikisha vyema kazi za Ofisi hiyo.
Mapema Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohammed Ali Ahmed alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo ambao aliahidi kuutumikia vyema.Naibu Msajili huyo ameahidi kutekeleza vyema majukumu yake ya kazi kwa kusimamia vyema sheria za vyama vya siasa nchini huku akieleza kuwa atahakikisha anatekeleza ipasavyo sheria hizo kwa lengo la kuwatumikia wananchi ili waweze kupata maendeleo sambamba na kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano mkubwa uliopo nchini.
Rais Dk. John Magufuli alimteua Mohammed Ali Ahmed tarehe 20 Juni 2018 ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mwanasheria na mtafiti katika Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar ambaye amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Rajab Baraka Juma ambaye amestaafu.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Diwani Athumani aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kujitambulisha kwa Rais.
Katika mazungumzo kati yake na kiongozi huyo, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuendeleza mashirikiano kati ya (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).Rais Dk. Shein alieleza kuwa licha ya taasisi hizo kwa kila moja kufanya kazi zake lakini bado zote zina kazi ya kupambana na kudhibiti rushwa na kusisitiza kuwa kupambana na rushwa na kusimamia maadili ya viongozi ni mambo ya msingi katika utawala bora ambapo iwapo yakifanywa vizuri yatawasaidia wananchi.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna wa Polisi Diwani Athumani alieleza kuwa suala la rushwa ni changamoto kubwa ambayo si kwa Tanzania tu bali ni dunia nzima.
Alisema kuwa rushwa inawagusa moja kwa moja wananchi wa kada zote hasa katika eneo la maendeleo hivyo mashirikiano ya pamoja yanahitajika katika kupambana nayo.Alisisitiza kuwa kumekuwepo mashirikiano makubwa kati ya Taasisi hiyo na ile ya Zanzibar ambapo miongoni mwa maeneo wanayoendelea kushirikiana ni pamoja na utoaji mafunzo na kubadilishana uzoefu.
Rais Dk. John Pombe Magufuli alimteua Kamishna wa Polisi Diwani Athumani kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mnamo Septemba 6, 2018 ambapo anachukua nafasi ya Kamishna wa Polisi Valentino Mlowola ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.