RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema uzinduzi wa vyumba vya madarsa ya skuli ya Sekondari Kijini, una mnasaba mkubwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015 – 2020.Amesema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Viongozi wa Chama hicho waliahidi kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ikiwemo uimarishaji wa sekta ya elimu,
Dk. Shein amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa vyumba vya madarasa manne (4) ya kusomea katika skuli ya Sekondari Kijini, Mkoa wa Kaskazini Unguja, yaliojengwa na Mwekezaji kutoka Kampuni ya “Andbeyond” inayomiliki Hoteli za kitalii za ikiwemo Mnemba Island Lodge ya hapa Zanzbar.
Ujenzi wa mabanda hayo ulioanza February 2018 hadi Octoba, 2018 umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 148.5 hadi kukamilika kwake, ikiwa pamoja na ununuzi wa samani za walimu na wanafunzi.Dk. Shein alimpongeza mwekezaji huyo na kusema ameonyesha njia kuelekea maendeleo ya kielimu nchini, sambamba na kuahidi Serikali kuendeleeza juhudi hizo ili kuimarisha sekta hiyo.Akigusia sekta ya elimu kabla ya Mapinduzi, Dk. Shein alisema hadi kufikia mwaka 1948, Zanzibar ilikuwa na skuli chache za msingi na sekondari, wakati ambapo Mkoa wa Kaskazini ulikuwa na skuli ya Mkwajuni pekee.
Alisema Wazanzibari wanyonge walishindwa kupata elimu, kwa vile ilikuwa ikitolewa kwa misingi ya matabaka na uwezo wa mtu.Aidha, alisema wananchi wa Nungwi walinyimwa haki ya kupata elimu baada ya kupotoshwa juu ya faida zake, sambamba na kuharibu utamaduni wao.Alisema Mapinduzi ya 1964 yalikuja kumkomboa Mzanzibari, baada ya elimu kutolewa bure, ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Chama cha ASP iliyowekwa wakati wa kupigania uhuru.
Alisema hivi sasa sekta ya elimu imeimarika nchini na imekuwa ikipatikana katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Shina, Wadi, Wilaya hadi Mikoa.
Alisema mnamo mwaka 2014, Serikali ilipanga kuandikisha wanafunzi wa elimu ya msingi kwa asilimia mia moja hadi kufikia mwaka 2020, jambo ambalo limetekelezwa kabla ya wakati, ambapo hivi sasa tayari wanafunzi walioandikishwa wamefikia asilimia 116 (116%), huku elimu ya sekondari wakifikia asilimia 86 (86%).Dk. Shein, alisema hivi sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa skuli tisa za Ghorofa katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, wakati ambapo kuna Vyuo Vikuu vitatu vya elimu yajuu, kimojawapo kikiwa cha Serikali.
Alisema lengo la serikali ni kuwaandaa wanafunzi ili kuwa na wataalamu katika fani tofauti, kwa lengo la kulisaidia Taifa pamoja na kuwasaidia wazazi wao.Alisema Jimbo la Kijini lina bahati kubwa, hivyo linapaswa kuendelea kuimarishwa kielimu, akibainisha matarajio yake katika kipindi cha miaka kumi ijayo ya jimbo hilo kupata Chuo Kikuu.
Aidha, Dk. Shein aliwataka wazee na wazazi wa kijiji hicho kuwa imara na kuwaelimisha watoto wao, sambamba na kuepuka upotoshaji na udanganyifu unaosambazwa na watu wasiowatakia mema.Katika hatua nyengine Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa Kijini na maeneo jirani kuwa barabara ya Mkwajuni – Kijini hadi Mbuyutende itajengwa mwaka ujao, mara tu baada ya barabara ya Bububu – Mkokotoni kumalizika ujenzi wake.Alisema maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vyema ,ambapo tayari serikali imeagiza vifaa vinavyohitajika na vyengine tayari vimeshawasili.
Mapema, Makamo wa Pili wa Rais wa Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, aliwataka wawekezaji wengine wenye miradi katika maeneo hayo kuiga mfano wa kampuni ya ‘Andbeyond’ ili kuisaidia jamii inayowazunguka.Alisema kuna wapo wawekezaji wengi katika maeneo hayo, hivyo akataka kutumia sehemu ya faida wanayopata kusaidia huduma za kijamii.“Kutokana na uwekezaji Serikali hunufaika kutokana na kupata mapato sambamba na wananchi kunufaika kutokana na faida kupitia sekta za kijamii kama vile upatikanaji wa huduma za maji, afya na barabara”, alisema.
Aliwataka wananchi hao kushirkiana na wawekezaji wa maeneo hayo ili hatimae waweze kunufaika na matunda yatokanayo na uwekezaji.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma aliishukuru Kampuni ya ‘Andbeyond’ kwa misaada mbali mbali inayotowa kwa wananachi wa maeneo hayo, ikiwemo uimarishaji wa sekta ya elimu.Alisema misaada hiyo inakuja kutokana na mazingira bora yaliowekwa na Serikali kupitia sekta ya uwekezaji na kutoa fursa kwao ya kuisaidia jamii.
Aliwataka wazazi kutumia vyema fursa zinazotolewa na serikali na kushirikiana nayo ili kufanikisha dhana ya uimarishaji wa sekta ya elimu hasa katika Mkoa huo.Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Madina Mjaka alisema ujenzi wa madarasa hayo utapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, hadi kufikia wanafunzi 45 kwa darasa moja.Aliwashajiisha wazazi na walezi wa maeneo hayo kuthamini juhudi zinazochukuliwa kwa kuandikisha wanafunzi wote wanaopasa kuanza masomo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa shukurani kwa kampuni iliyofanikisha ujenzi huo kwa juhudi kubwa iliyofanya, sambamba na kushirikiana vyema na wananchi wa eneo hilo.
Wakati huo huo, Dk Shein akiwa pia, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alifanya mazungumzo na Kamati ya siasa ya CCM Wilaya Kaskazini ‘A’, Viongozi wa ngazi mbali na wanachama katika Hoteli ya La Gemma Dell ‘Est’, Nungwi.Alisema Wilaya hiyo ni miongoni mwa zile zenye changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi, inayochangiwa na wananchi pamoja na baadhi ya viongozi.
Aliwataka wale wote wenye tabia hiyo kuacha vitendo hivyo, akibainisha kuwa vina athari kubwa katika ustawi wa sekta ya Utalii nchini.Aidha, Dk. Shein aliwataka wanachama wa chama hicho kujipanga vilivyo kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao wa 2020, sambamba na viongozi wa majimbo (Wabunge na Wawakilishi) kutumia kipindi kilichobaki kabla ya uchaguzi huo kutekeleza ahadi walizoweka kwa wananchi.
Akieleza azma ya Serikali anayoiongoza Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imedhamiria kuzitengeza kwa pamoja barabara za Mbuyu Maji na Mlilile kwa kuchelewa kwake kumetokana na kukosekana vifaa vya ujenzi ambavyo hivi sasa tayari Serikali imeshanunua na vyengine vimeanza kuwasili.Alieleza kuwa tayari lengo la Serikali la kufikishwa watalii 500,000 mnamo mwaka 2020 limeshavukwa kwani mwaka jana 2017 watalii walioitembelea Zanzibar walifikia 520,000.
Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wanaoishi Ukanda wa bahari katika Mkoa huo kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usala katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama ili liweze kwuavutia wageni wengi ambao wanapenda.