Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuunda Tume Maalum itakayofanya tathmini ya kina kuhusu fidia walizolipwa wananchi waliopisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya Fumba, Nyamanzi, Dimani na Bweleo, ili kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake stahiki.

Amefahamisha kuwa Tume hiyo itahakiki fidia zote zilizotolewa kwa wananchi na kujiridhisha ili kuhakikisha kila anayestahiki analipwa kwa mujibu wa sheria.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo, Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ametoa ahadi hiyo baada ya kusikiliza hoja za wananchi, ambapo wengi walieleza kutoridhika na fidia walizopokea baada ya kupisha miradi ya uwekezaji na maendeleo katika maeneo yao.Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Serikali kudhibiti watu wanaofanya udanganyifu wakati wa utekelezaji wa miradi kwa kujenga haraka au kuotesha miti ili walipwe fidia jambo ambalo halikubaliki kisheria.

Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali, na yeye binafsi, hawataridhia mtu yeyote kudhulumiwa, na kila mmoja atapata haki yake stahiki kwa mujibu wa eneo analomiliki.Ameeleza kuwa lengo la Serikali si kuwatia watu umasikini bali kuwaondolea umasikini, na amewaahidi wananchi kulipwa fidia stahiki mara baada ya Tume hiyo kukamilisha kazi yake ya tathmini.

Vilevile, amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kuandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutekeleza miradi yoyote ya maendeleo, pamoja na kupiga picha za maeneo husika ili kuweka kumbukumbu sahihi zitakazosaidia kuepusha migogoro.Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa awamu nyengine, ili aweze kukamilisha utekelezaji wa ahadi na kuleta maendeleo makubwa zaidi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Muhammed Said Dimwa, amesema Chama Cha Mapinduzi hakikukosea kumteua Dkt. Mwinyi kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar, kwa kuwa ni kiongozi anayejali wananchi, mtekelezaji wa ahadi zake na mwenye dira ya maendeleo ya kweli kwa taifa.

Wananchi waliopata nafasi ya kutoa hoja zao katika mkutano huo walimshukuru Dkt. Mwinyi kwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa ahadi zake zilizosaidia kuondoa changamoto nyingi za kijamii.