RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964 ndiyo yaliyoleta ukombozi hapa Zanzibar na yeyote aliyekuwa hayataki na anayabeza ni vyema akatafuta mahali akaenda.Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa soko la Kinyasini, lililopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 yameongeza fursa kwa wananchi ambao wote wamefaidika nayo na hakuna hata mwananchi mmoja wa Zanzibar aliyekwua hakufaidika na Mapinduzi.Mapinduzi yamefanyika kwa lengo la kuwapa hadhi Wazanzibari wote sambamba na kuwa huru kwani yameweza kuwakomboa watu wote wa Unguja na Pemba, shama na mjini.
Dk. Shein alieleza kuwa tangu Awamu ya Kwanza hadi leo hii, Awamu zote zinaendelea kuyaenzi, kuyatunza na kuyalinda Mapinduzi kwa nguvu zote sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza maendeleo yaliopatikana hivi sasa na yale yaliokuwepo kabla ya Mapinduzi na kuyafananisha hasa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu jinsi ilivyoimarika hivi sasa na ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 katika maeneo yote ukiwemo Mkoa wa Kaskazini.
Alisisitiza kuwa soko hilo ni la wananchi wote wa Kaskazini A, B kwa maisha yao pamoja na wananchi wengine wa mikoa mengine ambao watakwenda kufuata mahitaji sokoni hapo.