Makamo Mwenyekiti huyo ambaye pia, ni na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein aliyasema hayo, leo huko katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma wakati akiufunga Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM alisema kuwa CCM si chama kinachoshabikia mivutano, malumbano na misuguano kwani hayo yamezoeleka kusikia katika vyama vyengine vya kisiasa.
Dk. Shein alisema kuwa kukubaliana na matokeo ni tabia ya kiungwana na ndio utamaduni wa CCM, hivyo alitumia fursa hiyo kuwapongza wale wote ambao kura zao hazikutosha kwa kuyakubali matokeo, wakayapokea kwa mikono miwili na wanaaendelea kuwa waaminifu na kuwa pamoja na UVCCM na wana CCM wenzao kwa moyo mkunjuvu na moyo ule ule.
Alimpongeza Kheri Denis James kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa UVCCM Taifa na Tabia Maulid Mwita kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa. Aliutaka Umoja huo wa Vijana kutumia mitandao ya kijamii na hata majukwaa ya kisiasa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo, katika kutekeleza jukumu lao la kukilinda na kuitetea CCM.
Aliwahimiza kuzitumia mbinu bora zilizotumiwa na UVCCM ya miaka iliyopita ambayo ambayo ilijibu hoja kwa wakati, waliungana mkono mambo makubwa yalioamuliwa na chama wakati wote.
Alisisitiza suala la kuyazingatia maadili ya uongozi jambo ambalo limepewa umihumu mkubwa katika chama hicho na kueleza kuwa chama hicho kina historia ya kuwa na safu nzuri ya viongozo wanaojitambua, wanaowajali wanaowaongoza na kuzingatia kuwa cheo ni dhamana.
Alisema kuwa wagombea wasiozingatia mambo hayo hawapewi nafasi ndani ya chama hicho pamoja na Jumuiya zake katika chaguzi zake zote hivyo, UVCCM haiwahitaji viongozi wanaopatikana kwa mtindo wa rushwa na wanaoweka mbele maslahi yao binafsi. Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya vikao kwa Jumuiya hiyo kwa ajili ya kuzungumzia masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Chama na jamii kwa jumla.
Aliitaka Jumuiya hiyo kurudi kuwa kitu kimoja kwani uchaguzi umekwisha na waache kuendeleza makundi kwani yanaathiri nguvu ya umoja ndani ya CCM na kuwataka viongozi wapya kutambua kuwa nafasi hiyo waliopewa ni kwa ajili ya kuwatumikia wana UVCCM na CCM kwa jumla na si nafasi ya kutilia pozi, mbwembwe au kuonesha majigambo kwa watu wengine mitaani.
Dk. Shein aliwasisitiza viongozi wapya waliochaguliwa kipindi hiki wazingatie sana uwezo, maadili, uzalendo na sifa zilizopelekea kuchaguliwa kwao waendelee kuwa na sifa hizo katika kipindi chote cha miaka mitano na baadae kwani imeonekana kuwa baadhi ya viongozi wanaochaguliwa baada ya muda huanza kuyumba, wanakuwa wajuaji, hawaambiliki na hawakubali ushauri wa viongozi wao na wakubwa wao.
Aliwatahadharisha Wajumbe hao kuwa si busara kwa kiongozi katika kipindi kifupi baada ya kupata nafasi ya uongozi wa UVCCM ama CCM kuanza kuhaha kujitengenezea umaarufu ili apate cheo kikubwa ama fedha na mambo mengine.
Hivyo, aliwataka UVCCM wasikubali kuongozwa na watu wanaotaka kuwatumikia wawe mabosi wao kwa maslahi yao na wajue kuwa hao si viongozi wa UVCCM bali ni viongozi feki huku akiwataka kutofikiria makundi kwani chama kitayafyeka mapema pale yakibainika.
Nao viongozi waliochaguliwa walieleza matumaini yao na azma yao katika kuitumikia Jumuiya hiyo na kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja. Mapema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye ndie aliekuwa msimamizi wa uchaguzi huo alitoa matokea ya uchaguzi Mkuu huo wa UVCCM na kuwatangaza washindi wa uchaguzi huo.