Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inalizingatia kundi la vijana kuwa ni kundi maalumu lenye changamoto ambazo ni wajibu wa serikali kuzitafutia ufumbuzi.Aliyasema hayo katika uzinduzi wa matembezi ya jumuiya ya vijana wa chama cha Mapinduzi wa mikoa yote ya Tanzania, katika kiwanja cha mpira Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar matukufu ya Januari 12.1964.
Rais Dk. Mwinyi alisema, jitihada za Serikali ni pamoja na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi mbali mbali pamoja na kuboresha mafunzo ya ufundi wa fani tofauti kwa vijana wanaojiunga kwenye vyuo vya mafunzo ya amali.Alisema, hatua nyengine ni vijana kujiunga na mabaraza ya vijana yaliyoanzishwa katika Wilaya zote za Unguja na Pemba ambayo shughuli zake zinasimamiwa na kuratibiwa na wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo.
Aliongeza kuwa uwepo wa mabaraza hayo, ni jukwaa la kuwaunganisha vijana kubuni miradi ya kiuchumi na kuwapatia mitaji, taaluma na masoko ya kuuzia bidhaa zao. Hivyo nimatumaini yake kuwa mabaraza hayo yakiimarishwa vyema yatasaidia sana vijana kukabiliana na tatizo la ajira.Dk. Mwinyi alisema, ujenzi wa uchumi wa kisasa unaodhamiriwa kujengwa, unalengo la kuziendeleza jitihada za mafanikio ya awamu za uwongozi zilizotangulia, na kuelekeza nguvu ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi.Alisema, licha ya changamoto zilizotokana na athari za UVIKO-19 lakini Zanzibar imeanza kupiga hatua za kwenda ambako nchi imedhamiria, hivyo ni wajibu wa wananchi wote kuunga mkono na kushirikiana na serikali katika kuyafikia malengo.
Alisema, uwajibikaji, uzalendo na ushirikiano ni mambo ya msingi yatayowawezesha Wazanzibar kupiga hatua zaidi za kimaendeleo, na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili ikiwemo tatizo la ajira kwa vijana.“Mimi binafsi nimevutiwa sana na utaratibu huu wa kuwajumuisha vijana kutoka maeneo mbali mbali ya nchi yetu na kuwa pamoja katika masuala haya ya kuhamasishana uzalendo na umoja pamoja na kukumbushana masuala muhimu ya mustakbali wa taifa letu”, alisema.
Sambamba na hayo amesema sote ni mashahidi wa kuwa nchi yetu imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika kipindi cha miaka 58 ya Mapinduzi tokea kufuzu kwa mapinduzi yaliyoongozwa na waasisi walioongozwa na jemedari Mzee Abeid Amani Karume.Alieleza kwa jitihada zao viongozi waliotangulia pamoja na wananchi wa Kisiwa cha Unguja na Pemba, walifanya kazi kubwa ya kuijenga nchi yao na ndio hadi leo wananchi wanafurahia jitihada hizo hivyo alisema, ni wajibu wa kila mmoja kuziendeleza jitihada hizo kwa faida yao na kizazi kijacho.
“Nimepata faraja kuona hamasa kubwa walionayo washiriki wa matembezi haya kama hatua muhimu ya kuona kila mshiriki yupo tayati kuanza na kukamilisha matembezi hadi mwisho wake yatakapopokelewa na Rais wa Jamhuri ya Tanzania”, alisema.Alifahamisha kuwa, ni wajibu wa kila Mzanzibar kuyadumisha na kuyaendeleza matunda ya Mapinduzi katika kuimarisha uchumi wa kuwezesha hali ya kipato cha wananchi na ustawi wao kuendelea kuwa bora.
Aidha, alisema ni wajibu wa vijana kuendelea kuwa wazalendo, kudumisha amani, wachapakazi, watetezi wa amani umoja na mshikamano na walinzi wa mapinduzi matukufu ya Zanzibar na muungano wa Tanzania kwa nguvu zao zote.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisema, matembezi hayo ya UVCCM ni kielelezo thabiti cha kuonesha vijana wanalinda chama na Mapinduzi yao.“Ni vigumu sana kufahamu uzito walioupata wazee wetu wakati wa mapinduzi lakini leo vijana hawa sio kwa nadharia bali kwa vitendo wameonesha namna gani wazee wetu walipigana kwa ajili ya uhuru wan chi zetu”, alisema.
Kwa upande wake mlezi wa matembezi ya vijana wa UVCCM ambae pia ni Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Maryam Hussein Mwinyi alisema, matembezi hayo yanafaida kubwa kwa jamii na kuacha alama.“Nikiwa mlezi wa matembezi haya nakushukuru sana mgeni rasmi kwa kutufungulia matembezi yetu nasema asante sana kwa niaba ya wote, nawapongeza sana vijana kwa uwamuzi wao wa kufanya matembezi kila mwaka kuuwezi muungano wetu”, alisema.
Alieleza, safari hii vijana watakwenda kuitangaza na kuwaeleza vijana juu ya sera ya uchumi wa buluu kuunga mkono serikali ya awamu ya nane kupitia sera hiyo ambayo ni muhimu yenye lengo la kutatua suala la ajira kwa vijana.Mapema akitoa taarifa ya matembezi hayo Naibu katibu mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa alisema, vijana hao watatembea jumla ya km 124.9 ya mikoa yote ya Kisiwa cha Pemba.
Alisema, matembezi hayo ya siku tano yameanza rasmi mara baada ya kufunguliwa hadi kufikia kilele cha matembezi Januari 7 mwaka huu katika Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.Matembezi hayo yamewashirikisha vijana wa CCM zaidi ya 700 ambao watapita katika maeneo mbali mbali kufikisha ujumbe kwa jamii kuhimiza uhai wa chama na jumuiya zake na kuunga mkono juhudi za Serikali ya kudumisha Mapinduzi ya mwaka 1964 yakiwa na kaulimbiu isemayo “uchumi wa buluu ni fursa yetu vijana tuitumie”.
Katika uzinduzi huo pia, Rais Dk. Miwnyi alikabidhi picha za viongozi pamoja na bendera za Taifa kwa vijana watembeaji.