MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wanachama wa CCM kuchagua viongozi makini watakaoweza kukivusha Chama hicho katika Uchaguzi mkuu ujao wa 2025.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika Ukumbi wa CCM Kilimani, aliposhiriki katika mkutano mkuu wa Uchaguzi Ngazi ya Wadi ya Migombani, Jimbo la Mpendae, Mkoa Mjini Magharibi.

Amesema kazi kubwa ya Chama cha siasa ni kushika Dola, hivyo akawataka wajumbe wa mkutano huo kuwa makini na kufanya uamuzi sahihi wa kuchagua Viongozi bora watakaoweza kukivusha Chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Alieleza kuridhishwa kwake na hali ya mambo inavyoendelea katika mchakato wa chaguzi mbali mbali, kuanzia ngazi ya shina na Tawi na kusema zimetawaliwa na amani na usalama, hivyo akatoa wito kwa wanachama hao kuendeleza hali hiyo katika chaguzi zinazofuatia.

Alisema wakati Chama hicho kimekamilisha mchakato wa uchaguzi katika ngazi za shina na matawi (na sasa) Wadi, ni muhimu kuweka mazingatio katika chaguzi za ngazi za Jimbo, Mkoa na Taifa kutokana na ukubwa wa nafasi hizo.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi ametoa rambi rambi kwa Wazazi, Wanafamilia pamoja na wanachama wa CCM Tawi la Kilimani kutokana na kifo cha mwanachama wa CCM na mwanaharakati Suleiman Omar ‘Ommy Rey’ aliefariki dunia na kuzikwa jana katika makaburi ya Mwanakwerekwe Magharibi ‘A’ Unguja.



Aliwataka wanafamilia na wanachama hao kuwa na subra karika kipindi hiki kigumu pamoja na kumuombea marehemu huyo maghufira kwa Mwenyezi Mungu.

Nae, msimamizi katika Uchaguzi huo Haji Hassan Khamis ( Mwenyekiti wa Wazazi Jimbo la Amani) alisema jumla ya wanachama 74 wamejitokeza kupiga kura katika nafasi sita zinagombewa na wanachama kadhaa wa Chama hicho.

Alizitaja nafasi zilizogombewa kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Wadi nafasi moja, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wadi (nafasi 5) Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo (nafasi 5), Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa (nafasi 5), Katibu wa Wadi (nafasi 1) pamoja na Katibu Mwenezi wa Wadi nafasi moja.

Kufanyika kwa uchaguzi huo kunatokana na Kalenda ya Chama cha Mapinduzi, ambapo Viongozi wanaochaguliwa wataendelea kushika nyadhifa hizo hadi ifikapo mwaka 2026.

Hafla hiyo ya Uchaguzi ilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma ‘Mabodi’, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Idrissa Kitwana Mustafa pamoja na Viongozi mbali mbali wa chama hicho ngazi za Mkoa na Wilaya