RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la   Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi amemuapisha Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla pamoja na Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia uteuzi aliofanya Juni 24, 2022.Katika hafla hiyo iliofanyika Ikulu Zanzibar, Dk. Mwinyi aliwaapisha kushika nyadhifa hizo Jaji Said Hassan Said, Jaji Salma Ali Hassan pamoja na Jaji Mohamed Ali Mohamed kuwa Majaji wa Mahakama Kuu Zanzibar.

Kabla ya Uteuzi huo Jaji Mkuu Khamis Ramadhan Abdalla alikuwa anakaimu wadhifa wa Jaji Mkuu wa Zanzibar, wakati ambapo Jaji Salma Ali Hassan alikuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP).Aidha, Jaji Mohamed Ali Mohamed alikuwa Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar na Jaji Said Hassan Said alikuwa Mwanasheria Mkuu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba.

Wakizungumza baada ya hafla hiyo ya kiapo, Majaji hao waliahidi kusimamia kikamilifu majukumu ya kazi zao ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki anayostahili kwa mujibu wa sheria za nchi.“Nitaweka kipaumbele ili kuhakikisha kesi za udhalilishaji na dawa za kulevya zinashughulikiwa kwa haraka ili kuhakikisha aynakabidhiwa”, alisema Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla.

Aidha, Majaji hao walitoa wito kwa wananachi kuondokana na muhali na kufika Mahakamani kutoa ushahidi wa mashauri mbali mbali yanayowasilishwa, ikiwemo yale ya udhalilishaji na dawa za kulevya.Katika hafla hiyo, viongozi mbali mbali wa Kitaifa walihudhuria, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Mwinyi Talib Haji, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said.
Wengine ni pamoja na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wanafamilia.