RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amemuapisha bi Khadija Khamis Rajab kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Viwanda.

Hafla hiyo iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar ilihudhuriwa na Viongozi mbali mbali, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said na Naibu Waziri Wizara ya Biashara na Viwanda Hassan Khamis Hafidh.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Kadhi Mkuu Sheikh Othman Ngwali, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahamoud, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Washauri wa Rais wa Zanzibar, viongozi wa serikali pamoja na wana familia.

Nae, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Khadija Khamis Rajab, alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kumuamini na kumkabidhi wadhifa huo kwa maslahi ya Taifa.

Aliahidi kufanya kazi zake kwa juhudi kubwa na kufuata miongozo na sheria zilizopo ili kuharakisha kasi ya kuliletea Taifa maendeleo.

Aidha, aliahidi kufanya kazi kwa mashirikiano makubwa na wafanyakazi wa Wizara hiyo pamoja na viongozi wa serikali ili kuleta ufanisi.