RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza mazishi ya Marehemu Ali Ferej Tamim huko katika Makaburi ya Mwanakwerekwe mjini Unguja na kuungana na ndugu, jamaa,marafiki pamoja na wanamichezo mbali mbali walioshiriki mazishi hayo.

Marehemu Ali Fereji Tamim ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa Chama Cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kwa zaidi ya miaka 20 na kukiongoza chama hicho katika nyadhifa mbali mbali ikiwemo Urais wa Chama hicho.

Aidha, Marehemu Ali Ferej Tamim ambaye ni mmoja wa wanamichezo waliotoa mchango mkubwa katika mpira wa miguu hususan Zanzibar pia, aliwahi kushika wadhifa wa kuwa Makamo wa Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa muda mrefu.

Sambamba na hayo, Marehemu Ali Ferej Tamim alichukua juhudi kubwa katika uongozi wake katika kuhakikisha Zanzibar inapatiwa uwanachama wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) pamoja na kuhakikisha ligi kuu ya Zanzibar inapata udhamini na kuvipa nafasi vilabu vidogo vidogo.

Ali Ferej Tamim amefariki dunia leo alfajiri katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu ambapo Marehemu Ali Ferej ameacha kizuka mmoja na watoto wawili.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein pia, alishirikia mazishi ya Marehemu Bi Mansab Masoud hapo hapo katika makaburi ya Mwanakwerekwe ambapo mapema aliungana na ndugu na jamaa pamoja na Waislamu katika sala ya kumsalia Marehemu Bi Mansab katika msikiti wa Jaamiu Zinjibar, uliopo Mazizini mjini Unguja.

Mapema Rais Dk. Ali Mohamed Shein, alifikika Uzini, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusni Unguja kwa ajili ya kutoa mkono wa pole kwa familia ya Marehemu Maalim Ramadhani Abdalla Shaaban na kuitaka familia hiyo kuwa na subira hasa katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Salamu hizo za pole za Rais Dk. Shein alizitoa kijijini huko mara tu baada ya kufika akirejea kisiwani Pemba, na kuitaka familia hiyo kuwa na moyo wa subira na kuendelea kumuombea dua Marehemu.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumuelezea Marehemu Maalim Ramadhan Abdalla Shaaban kwa ufupi kwa namna walivyokuwa pamoja katika uhai wake tokea wakati wakiwa wanafunzi na wakati wakiwa wafanyakazi Serikalini pamoja na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, Rais Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu aipe moyo wa subira familia hiyo na kumuomba Mwenyezi Mungu kuilaza mahala pema peponi, roho ya Maremu Maalim Ramadhan Abdalla Shaaban.

  • RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiwafariji na kutowa mkono wa Pole kwa Wajane wa Marehemu Ramadhan Abdalla Shaban, aliofika Kijiji kwao Uzini leo kutowa mkono wa pole kwa familia.RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiwafariji na kutowa mkono wa Pole kwa Wajane wa Marehemu Ramadhan Abdalla Shaban, aliofika Kijiji kwao Uzini leo kutowa mkono wa pole kwa familia.