RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Futari hiyo imeandaliwa na Alhaj Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba ilifanyika katika Ikulu ndogo Chake Chake, ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa, Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa huo.

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nae alishiriki kikamilifu katika hafla hiyo ya futari akiwa pamoja na viongozi wanawake wa Kitaifa na wananchi wengine wa Mkoa huo.Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais Dk. Shein, Mkuu wa Mkoa huo Hemed   Suleiman Abdalla aliwataka wananchi kuendeleza amani, utulivu, umoja na mshikamano pamoja na kuendelea kuiombea dua nchi yao ili iendelee kupata neema.

Alieleza kuwa mafanikio makubwa yataendelea kupatikana hapa nchini iwapo mashirikiano ya pamoja yatakuwepo na wananchi wote wataendelea kuwa kitu kimoja.Alieleza kuwa nafsi zote zikiwa pamoja basi Mwenyezi Mungu ataendelelea kuleta neema na kuwasisitiza wananchi Waislamu na wasiokuwa waisilamu kuendelea kuiombea dua nchi, viongozi pamoja na kuwaombea wananchi wote.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kutoa mashirikiano wakati wote kwa shughuli zote za Serikali na za kijamii kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao.Sambamba na hayo, aliwataka wananchi kuendelea kupiga vita vitendo vyote viovu kwa maslahi yao pamoja ili jina la Zanzibar liendelee kutajika vyema.Alitoa shukurani kwa wananchi wote waliofika katika kufutari pamoja kwa kuungana na Rais Dk. Shein kwa ajili ya kufanya kitendo hicho cha ibada hasa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwashukuru wananchi pamoja na viongozi wote wa dini na vyama vya siasa waliohudhuria katika futari hiyo aliyowaandalia na kupongeza jinsi walivyoonesha upendo mkubwa kwake wa kukubali muwaliko wake huo.

Mkuu huyo wa Mkoa pia, alimpongeza Alhaj Dk. Shein kwa kitendo chake hicho cha kufutarisha na kueleza fadhila na ujira mkubwa anaopata mtu anaefutarisha wenziwe na thamamani ya kufutarisha.Pia, walimuombea dua Alhaj Dk. Shein kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa amani na utulivu na kumuomba Mwenyezi Mungu ili kiongozi huyo aendelee kuwafanyia mazuri kama aliyowafanyia ambapo yote hayo yatakuwaja iwapo wote watakuwa wamoja.

Nao wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba wakitoa neno la shukurani lililotolewa na Sheikh Mohammed Suleiman kwa niaba yao walitoa shukurani kwa futari nzuri aliyowaandalia na kuonesha furaha yao kwa kufutari pamoja kiongozi wao huyo.Kwa niaba ya wananchi hao, Sheikh Mohammed alieleza kuwa watu wema wanajuana kwa alama njema na Alhaj Dk. Shein ana alama njema kwani kuna dalili zote kuwa yeye ni Mcha Mungu, mnyeyekevu na amekuwa akimuogopa Mwenyezi Mungu pekee yake.Sheikh Mohammed alieleza kuwa ni neema ya kuwa na kiongozi kama huyo huku akitumia fursa hiyo kumuombea dua ili Alhaj Dk. Shein aendelee kuwa na afya njema.

Aidha, alieleza kuwa Alhaj Dk. Shein amekuwa karibu sana na raia wake na amekuwa haangalii wapi anapotoka ama kabila alilonalo na badala yake amekuwa akiwasaidia wananchi wake wote bila ya kinyongo wala ubaguzi.Sheikh Suleiman alimsifu Rais Dk. Shein kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo kwa kufanya kitendo hicho cha kuwafutarisha katika kumi hili la mwisho la Ramadhani ambalo linaubora na umuhimu mkubwa katika suala zima la ucha Mungu.

Leo Rais Dk. Shein anatarajiwa kufutari pamoja na wananchi wa Jimbo la Mkanyageni huko katika viwanja vya skuli ya Mkanyageni.