RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza mazishi ya marehemu Taimour Saleh Juma yaliyofanyika huko Kianga, Wilaya ya Magharibi ‘A’, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Viongozi mbali mbali wa vyama na serikali walihudhuria akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Kharib Billal na wengineo.
Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Taimour Saleh Juma huko katika Msikiti wa Ijumaa Mchangani Mjini Unguja.
Katika uhai wake marehemu Taimour aliwahi kushika nafasi mbali mbali za uongozi ikiwa ni pamoja na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalum, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko pamoja na nafasi nyengine za uongozi wa Serikali.
Pia, Marehemu aliwahi kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Makadara ambapo kabla ya nafasi hizo za uongozi aliwahi kuwa Meneja wa Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ.
Marehemu Taimour amezaliwa Disemba 1938 huko Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba, Marehemu ameacha watoto wanane na kizukaa mmoja, Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.