RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewasili mjini Dodoma leo kwa ajili ya kuhudhuria Sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.Katika uwanja wa ndege wa Dodoma, Rais Dk. Shein alipokewa na viongozi mbali mbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Bilneth Mahenge.Sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika kesho mjini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. John Pombe Joseph Magufuli.
Aidha, Sherehe hizo zinatarajiwa kuanza saa tatu asubuhi mara baada ya kuingia wananchi, wageni waalikwa pamoja na viongozi wa Kitaifa katika uwanja huo ambapo Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili saa tatu asubuhi uwanjani hapo. Baada ya kuwasili kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Gwaride litatoa salamu ya Rais na mizinga 21 kupigwa, wimbo wa Taifa na wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utapigwa na kuimbwa.
Baada ya tukio hilo, Kamanda wa Gwaride atamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu ambapo atakagua gwaride na baada ya hapo gwaride litasonga mbele kwa heshima na kutoa salamu ya Rais na Salamu ya Utii kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.Pia, Gwaride hilo litapita mbele kwa mwendo wa haraka na baadae litatoka uwanjani na kufuata onesho la kikundi cha Komando, onesho la bendi na onesho kutoka Jeshi la Magereza na Halaiki vitafuata.
Katika sherehe hizo pia, vikundi maalum vya ngoma za asili vitatumbuiza, Kwaya ya pamoja kutoka JWTZ, JKT, Polisi na Magereza navyo vitatumbuiza na baada ya hapo salamu kutoka kwa Mgeni Rasmi zitafuata ambapo baada ya kumaliza kwa salamu hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano ataondoka uwanjani na viongozi wengine wa Kitaifa nao wataondoka uwanjani.
Rais Dk. Shein, katika hotuba zake mbali mbali amekuwa akiahidi kuwa atauendeleza, ataudumisha na kuusimamia vyema Muungano uliopo kwa mashirikiano kati yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.Dk. Shein amekuwa akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuuimarisha Muungano uliopo.
Rais Dk. Shein amekuwa akieleza kuwa yeye na Rais Dk. John Pombe Magufuli wanatambua uzito wa dhamana waliyopewa na wananchi katika kuhakikisha kuwa Tanzania,inadumu na inaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wa Awamu zilizotangulia.Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein amekuwa akiwahakikishia wananchi kwamba Serikali zote mbili zitaendelea kuchukua hatua ili Tanzania iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na ibaki kuwa nchi ya amani na utulivu.