SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti katika kukuza michezo kwa kuendeleza vipaji vya watoto,kuimarisha mashindano na ligi za michezo mbali mbali pamoja na kuekeza katika miundombinu ya michezo hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo katika harambee iliyofanyika kwa ajili ya kutekeleza Mpango mahsusi wa kuimarisha michezo katika skuli Ports 55, huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi.
Katika hotuba yake, aliyoitoa mara baada ya kufanyika harambee iliyokwenda sambamba na mnada wa picha maalum zikiwemo za Dk. Shein ambapo TZS milioni 367.8 zimechangwa zikiwemo fedha taslim TZS milioni 77.2 na fedha za ahadi TZS milioni 226.1 na vifaa vyenye thamani ya TZS milioni 64.5.
Dk. Shein aliieleza imani yake kuwa Mpango huo wa Sport 55 utakuwa na mchango mkubwa wa kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto.
Alieleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kujenga viwanja vya michezo kwa kila Wilaya, ambapo tayari zoezi hilo limeshaanza.
Dk. Shein alieleza lengo la Serikali kuwafanya vijana wawe na upeo mpana zaidi wa kufahamu na kuipenda michezo ili waweze kujiamini na matumaini ya kuwa nyoya katika miaka michache ijayo.
Alisisitiza kuwa iwapo watoto watapewa mafunzo na mbinu za kisasa za michezo tangu wakiwa wadogo, wanaweza kuinuka na kuwa wanamichezo wa kilipwa wa kimataifa watakaotajika na kupendwa duniani kote.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa dhamira ya kuongeza kasi katika michezo hapa Zanzibar ina lengo la kuona namna Zanzibar inavyoirejesha hadhi ya michezo kwa kupata mafanikio makubwa katika Nyanja hii muhimu hasa katika wakati huu uliopo.
Dk. Shein alieleza kuwa michezo ni gharama na michezo ni sayansi kwani nchi nyingi zinazofanikiwa katika michezo ikiwemo mpira wa miguu ni zile zilizowekewa umuhimu mkubwa wa michezo maskulini, ikiwa ni pamoja na
kujenga vituo vya kufundishia michezo na kujenga miundombinu ya michezo.
Aliongeza kuwa michezo ina umuhimu mkubwa katika kuitangaza Zanzibar kiutalii na kibiashara.
Alisema kuwa katika jitihada za kufufua michezo,Serikali imeamua kuanzisha mpango wa Sport 55, ambapo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa miaka mitano ulioandaliwa na Serikali kwa ajili ya kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa lengo kuu la Mpango wa Sport 55 ni kuandaa mazingira mazuri kwa wanafunzi ili washiriki katika michezo.
Mapema Mwenyekiti wa Mpango wa 55, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa alieleza kuwa Mpango huo utasaidia kufufua michezo kwa vijana walio wadogo ambao wanatakiwa kuwa wakakamavu sambamba na kuibua vipaji.
Nae Waziri wa Elimu na Vyuo vya Amali Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa azma yake ya kuimarisha sekta ya michezo hapa nchininhasa kwa kuazia na vijana.
Hafla hiyo ilienda sambamba na taarab maalum ya Kikundi cha Taifa ambacho huwahusisha waimbaji mahiri kutoka Unguja na Pemba, ambapo taarab hiyo ilikonga nyoyo za watu kutokana na nyimbo mbali mbali zilizoimbwa na wasanii mahiri.
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mama Mwanawema Shein pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali, wafanyabiashara, watendaji wa serikali na wananchi.