RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakumbusha wananchi wa Zanzibar umuhimu wa kulinda na kuyaendeleza Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwa kuwa yalilenga kuwakomboa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba ili wawe huru .

Dk. Shein ambae pia ni Makamo Mwenyekti wa CCM Zanzibar, amesema hayo katika muendelezo wa Kampeni za chama hicho kwa Mkoa wa Magharibi Kichama, zilizofanyika Dole Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja.

Amesema kabla ya Mapinduzi ya 1964, wananchi wanyonge wa Zanzibar walidharauliwa, kupuuzwa na kubezwa katika nyanja zote na kubainisha kuwa kufanyika kwa Mapinduzi hayo kuliazimia kuwaweka pamoja na kushikamana.

Alisema hakuna mbadala wa Mapinduzi hayo na hivyo akawataka wananchi wayatunzwe na kuyadumisha, akibainisha watu wote kuwa ni sawa.

Alisema amani, umoja na mshikamano uliopo hapa nchini umeletwa na Mapinduzi na hivyo kutowa fursa za upatikanaji wa haki na fursa mbali mbali, ikiwemo matibabu bora,upatikanaji wa ardhi na kadhalika.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema hivi sasa wameibuka baadhi ya watu wanaotumia kisingizio cha siasa na kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani na ukatili kwa wananchi wenzao.
 
Alieleza kuwa CCM ni chama cha amani chenye sera na viongozi bora pamoja na kutekeleza vyema Ilani yake, huku akibainisha uteuzi bora wa wagombea wake kuelekea uchaguzi na hivyo akawataka wananchi na wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi Oktoba 28, 2020 na kuwapigia kura wagombea hao.

Alieleza kuwa Serikali ya CCM inaongozwa kwa misingi ya Katiba, na hivyo akabainisha jukumu kubwa walilonalo wanachama wake, la kuwapigia kura wagombea ili kukiwezesha kuendesha Dola, jambo alilosema ndio lengo la Chama hicho.

Nae, Mgombe wa kiti cha Urais kupitia CCM, ambae pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi alisema Serikali ya awamu ya nane itawangalia kwa karibu wafanyakazi wa sekta ya umma katika suala zima la kuboresha mishahara na posho zao.

Alieleza ili kufanikisha dhamira hiyo Serikali inakusudia kujiimarisha kiuchumi na kuwataka wafanyakazi kila mmoja mahala alipo kuwajibika ipasavyo katika kazi.

Aidha, Dk. Hussein alisema katika dhamira hiyo hiyo ya kukuza uchumi, serikali atakayoiongoza (pale atakapochaguliwa)  itapitia Pencheni za wastaafu kwa lengo la kuiboresha.

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya saba chini ya Uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein kwa kufanya kazi kubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.

Alisema miongoni mwa mafanikio yaliopatikana katika utekelezaji huo katika Wilaya zote za Mkoa huo ni uimarishaji katika sekta za Elimu, Afya, Miundombinu ya barabara pamoja na uaptikanaji wa huduma za maji safi na salama.

Alisema sekta ya Afya imefanyiwa kazi kubwa , ambapo vituo mbali mbali vya mama na mtoto pamoja na vya kujifungulia vimejengwa na kuimarishwa.

Aidha, alisema Serikali ijayo ya awamu ya nane inalenga kukamilisha kazi iliobaki ya kuondoa miundombinu ya maji iliochakaa na kuweka miundombinu mipya pamoja na kusambaza katika maeneo ambayo hivi sasa haipo.

Akigusia upande wa Ajira, Dk. Hussein Mwinyi alisema kila mwananchi anaehitaji kufanyakazi atapata fursa ya kufanya hivyo, akibainisha mpango wa serikali wa ajira 300,000, zikiwemo zilizo rasmi, zisizo rasmi pamoja na vijana wengine kuwezeshwa kimafunzo ili kuweza kujiajiri.

Katika hatua nyengine, Dk. Hussein alisema Serikali ijayo itasimamia utaifa na kuondokana na ubaguzi wa matabaka katika aina zote, iwe wa kidini au majimbo.

Vile vile alisisitiza umuhimu wa wananchi na wanachama wa CCM kuendelea kuilinda amani iliopo pamoja na kuwataka kuwa watulivu na kuviachia vyombo vya Dola kufanya shughuli zao.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Abdalla Juma Sadalla alisema katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2015-20020, viongozi wote wa Chama hicho walifanikiwa kushuka hadi ngazi za chini (ngazi za shina na matawi) na kusimamia utekelezaji wa Ilani hiyo.

Aidha, alisema Chama hicho kinalaani vikali vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyofanywa na baadhi ya wafuasi wa chama cha upinzani, na kuwasihi wanachama wa CCM kutolipiza kisasi.

Katika mkutano huo viongozi mbali mbali wa Kitaifa walishiriki, akiwemo Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali iddi, Waziri Kiongozi mstaafu Shamsi Vuai Nahodha pamoja na wake wa Viongozi wakuu.