MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alikutana na Mabalozi wa Wilaya ya Kaskazini Kaskazini B katika ukumbi wa CCM Mkoa uliopo Mahonda na kuwaeleza Mabalozi hao haja ya kuendeleza amani, umoja na mshikamano ambayo ndio Sera ya CCM. Katika mkutano huo ambapo pia, Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM aliongeza kuwa suala la amani, utulivu na mshikamano si la nadharia bali ni la vitendo kwa kutambua kuwa hakuna mbadala wa amani.
Aidha, Dk. Shein aliwaeleza Mabalozi hao hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji, umeme, barabara na mengineyo huku akisisitiza kuwa Serikali itachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha inawaajiri vijana kwenye sekta ya afya hasa wale waliosoma katika vyuo vya hapa Zanzibar. Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo leo katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Uguja uliopo Mahonda, Wilaya ya Kaskazini B, wakati alipozungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Kaskazini B Unguja ambapo pia, Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria.
Nao Mabalozi wa Wilaya hiyo, katika taarifa yao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kusimamia vyema Ilani ya CCM kwa vitendo na kutumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa kijiji cha Mgonjoni kwa namna alivyokifanya kijiji hicho kuwa mji wa kileo na kueleza kuwa malipo yao ni kuipa ushindi CCM katika uchaguzi wa mwaka 2020. Aidha, walitoa pongezi kwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, suala ambalo linawapunguzia utendaji kazi na kuondoa maadili ya watu wa Kaskazini.
Waliongeza kuwa wako pamoja na Makamo Mwenyekiti huyo kuwafichua wadhalilishaji wa kijinsia na kuiomba Serikali kutopunguza kasi katika kukemea kadhaa hiyo na kuwachukulia hatua stahili tena kwa wakati wahusika wote wa vitendo hivyo. Sambamba na hayo walieleza kuwa muda wa uongozi wake ni mdogo na mambo aliyoyafanya ni mengi kiasi kwamba hawawezi kuyaandika na kuyasoma kwa mara moja, mafanikio yanayotokana na juhudi za CCM katika kuihamasisha na kuisimamia Serikali na wananchi wake.