RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Rwanda Paul Kagame kwa ushindi  mkubwa alioupata kufuatia uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Agosti 4, mwaka huu. 

Katika salamu hizo za pongezi Dk. Shein alimpongeza Rais Kagame kwa ushindi wake huo uliompelekea kuendelea kuiongoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu, ushindi ambao umeonesha wananchi wa Rwanda jinsi walivyofarajika na uongozi wa Rais Kagame.

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Rwanda wameweza kuishuhudia nchi yao ikipata maendeleo makubwa pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu chini ya uongozi wa Rais Kagame katika vipindi vyake viwili vya uongozi.

Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Kagame kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Rwanda sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa Rwanda na wananchi wa Zanzibar.

Hivyo, Dk. Shein alimtakia uongozi mwema kiongozi huyo wa Taifa la Rwanda pamoja na kuendeleza maendeleo endelevu yaliopatikana nchini humo.

Rais Kagame mwenye umri wa miaka 59 alichaguliwa tena kuwa Rais wa Rwanda baada ya kuibuka mshindi katika kinyanganyiro cha kuwania urais kwa silimia 98.7 ya Kura na kuapishwa Agosti 18, mwaka huu.

Kuapishwa kwa Kagame kumekuja baada ya kupata ushindi huo kutokana na  kuwashinda wapinzani wake Frank Habineza kutoka Chama cha Kijani na Philippe Mpayimana ambaye alikuwa mgombea huru.