Ndugu Wananchi,
Assalam Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh
Alhamdu Lillahi Rabil Alamin. Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa Viumbe vyote. Sala na salam zimshukie Mtukufu wa Daraja, Mtume Muhammad (SAW) aliyeletwa kwa Rehema za Muumba wetu kwa ajili ya kuwaongoza waja katika kheri, ili wapate nusra ya Allah (Subhanahu Wataala).
Ndugu Wananchi,
Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, kwa kutujaaliya umri na kutuwezesha kwa mwaka mwingine kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Huu ni mwezi wa Ibada, mwezi wa Furaha, mwezi wa Neema na mwezi wa Toba. Miongoni mwa mambo makubwa zaidi katika mwezi huu ni kwamba, Allah alituteremshia Quran, Kitabu chenye hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Subhaanahu wa Taala alimwambia Mtume wake Muhammad (SAW) katika Surat Ibrahim aya ya kwanza katika tafsiri isemayo:
“Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako, ili uwatoe watu kwenye kiza uwapeleke kwenye mwangaza kwa idhini ya Mola wao, uwafikishe kwenye njia ya Mwenye Nguvu na Msifiwa”.
Vile vile, ndani ya Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, Mola wetu Mlezi amejaaliya usiku wenye cheo wa Laylatul Qadri ambao ni bora kuliko miezi elfu.
Kutokana na umuhimu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni wajibu wetu sote kuukaribisha kwa furaha, matumaini na kujiandaa kuzidisha kufanya ibada kwa wingi, ili tuweze kunufaika na fadhila za mwezi huu. Napenda nitoe risala hii kwa lengo la kuukaribisha na kukumbushana baadhi ya mambo tunayostahiki kuyafanya katika Mwezi huu Mtukufu. Madhumuni ya kukumbushana ni tuweze kufanikiwa hapa duniani na akhera twendako. Mwenyezi Mungu ametupa maelekezo kamili ya Mwezi huu katika Quran tukufu, Surat Al-Baqara aya 183 hadi 187, aya ambazo Mashekhe na Maimamu wetu wamezitilia mkazo na kuzielezea tangu ulipoanza mwezi wa Rajab hadi leo.
Vile vile, wakati tunapoukaribisha mwezi wa Ramadhani, tukumbuke kuwa kuna wenzetu ambao Ramadhani iliyopita tulikuwa pamoja nao, lakini tayari hatunao tena hapa duniani kwani wameshafika mbele ya haki. Sisi tulio hai tumshukuru Mola wetu kwa kutufikisha hadi leo na tunamuomba Mwenyezi Mungu atufikishe katika Ramadhani nyengine zijazo. Vile vile, tuzidishe kuwaombea kwa Allah wenzetu waliotangulia mbele ya haki, awarehemu, awaghufirie makosa yao na sisi atuzidishie subira na uwezo, wa kuzitekeleza ibada ndani ya Mwezi huu na miezi mingine kama alivyotuamuru.
Ndugu Wananchi,
Tunahimizwa kujiandaa na Ramadhani kwa kufanya zaidi mambo mema na ibada za Saumu, Sala na utoaji Sadaka katika mwezi huu wote. Vile vile ni wajibu wetu, kuzidisha kuisoma Quran na kuielewa pamoja na Hadith za Bwana Mtume Muhammad, S.A.W, ili tuweze kuzitekeleza ibada zetu vizuri. Tuhudhurie kwa wingi katika darsa, ili tuweze kupata elimu na maarifa ambayo yatatuongoza katika kufanya ibada zetu kwa usahihi zaidi. Mwenyezi Mungu ametuhimiza kusoma, ili tuyafahamu tusiyoyajua. Katika Suratul Alaq, aya za mwanzo, Mwenyezi Mungu ametusisitiza kusoma katika tafsiri isemayo:
“Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako ni Karimu sana. Ambaye amemfundisha binadamu elimu kwa msaada wa kalamu. Amemfundisha mwanaadamu mambo aliyokuwa hayajui”
Ni dhahiri kuwa, kuongeza juhudi katika kuisoma Quran na kuyazingatia mafundisho yake kutatuwezesha kukua kwa imani zetu na kumjua zaidi Mola wetu, ili kupata twaa ya kujiweka mbali na makatazo yake, ili tuweze kufanikiwa hapa duniani na kesho akhera.