RAIS wa Zanzibar naMwenyekitiwaBaraza la Mapinduzi Dk. Ali MohAmedShein,amewataka wadau wanaotunza na kusimamia rasilimali za ardhi kufanyakazi kwa uzalendo kwa kuzingatia misingi ya uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.

Dk Shein amesema hayo wakati alipofunga semina ya Kitaifa kuhusu masuala ya Ardhi na Rasilimali zisizorejesheka, iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni Mjini hapa.

Semina hiyo ya siku moja, iliwashirikisha Viongozi na Watendaji kutoka Wizara, Idara na taasisi za Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya ardhi.

Alisema ni muhimu watendaji hao kufanyakazi zao kwa kuzingatia misingi ya uzalendo, kwa kutambuwa kuwa rasilimali za ardhi na mali zisizorejesheka, ni nyenzo muhimu katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa.

Alisema kuna umuhimu wa kukumbushana juu ya dhana ya uzalendo miongoni mwa Wazanzibari ikiwa ni miongoni mwa mambo yaliopewa kipaumbele tangu wakati wa Mapinduzi.

Aliwataka wadau hao kutafakari na kudurusu sheria za ardhi zilizopo, akibainisha kuwa bado Taifa halijachelewa katika azma yake ya kutunza na kusimamia rasilimali hizo.

Aidha, Dk. Shein alisistiza umuhimu wa kuimarisha umoja, mshikamano na kufanyakazi kwa nidhamu, akibainisha kuwa hiyo ndio njia sahihi kuelekea mafanikio.

Mapema, washiriki wa semina hiyo waliiomba Serikali kujidhatiti vilivyo ili kukabiliana na vitendo vya uvunjaji wa sheria za ardhi, badala ya kukimbilia mahakamani kwa lengo la kuwadhibu wakosaji.

Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakari alisema sheria ziliopo ni nzuri, ila kinachokosekana kwa sasa ni uzalendo miongoni mwa watendaji na wasimamizi wa sheria za ardhi.

Alisema Serikali inadhima ya kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza na kusimamia sheria hizo na kubainisha kuwa hatua hiyo itaifanya jamii kusimama kidete katika ulinzi wa rasilimali za ardhi.

“Tutowe elimu kwa wananchi ili tulete uzalendo, kama mchanga umechimbwa hauwezi kurudi tena na kama muwembe umekatwa hauwezi kurudi…………..tuwe wazalendo kulinda sheria zetu, tusikimbilie mahakamani…………”, alisema.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa serikali, Said Hassan Said alisema changamoto zilizopo juu ya uharibifu wa rasilimali ya ardhi zinatokana na serikali kushindwa kuchukuwa hatua za kisheria dhidi yawakosaji kama zilivyobainishwa katika sheria na Katiba ya nchi.

“Anaetakiwa kuilinda na kuihifadhi ardhi hii kwa mujibu wa sheria na Katiba ni kila Mzanzibari”, alisema.

Alisema endapo taratibu za kutambuliwa ardhi,kupimwa,kusajiliwa au kuhaulishwa kisheria zitafuatwa, hakuna sababu ya kuwepo kwa changamoto za ardhi nchini.

Nae, Mohamed Adamu Makame, Kadhi wa Wilaya ya Mkoani Pemba, alisema pamoja na kuwepo sheria kadhaa za ardhi zilizo bora, lakini tatizo kubwa liliopo ni usimamizi wa sheria zenyewe.

Alisema ukataji ovyo wa miti kupitia misumeno ya moto pamoja na misitu unatokana na utendaji usiozingatia sheria katika ngazi za shehiya pamoja na Idara ya Misitu na maliasili zisizorejesheka.

Alisema kuna haja kwa Serikali kuifanyia marekebisho sheria ya ardhi inayohusiana na ugavi wa eka tatu ili kwenda sambamba na mahitaji ya wakati uliiopo, akieleza ongezeko kubwa la watu nchini linachangia baadhi ya maeneo ya ardhi kutumiwa kwa shughuli za ujenzi wa makaazi ya binadamu.

Aidha,Said Soud (Waziri asie na Wizara maalum wa SMZ) alisema kwa miaka kadhaa kumekuwepo upotoshaji wa sheria, ikiwemo ya ardhi kunakotokana na kauli za viongozi wa kisiasa hivyo kusababisha wananchi kuvunja sheria hizo.

Alisema iko haja ya kutunga sheria madhubuti za ardhi kwa mustakbali mwema wa vizazi vilivyopo na vijavyo na kubainisha kuwa hatua hiyo itapunguza migogoro na kesi katika mahakama ya Ardhi.

Nae, Hamad Rashid Mohammed (Waziri wa Afya) alisema changamoto zinazohusiana na rasilimali za ardhi nchini, zinatokana na usimamizi duni wa sheria, hivyo akataka elimu itolewe kwa jamii kuanzia ngazi za shuleni.

Alisema kumekuwepo udhaifu katika utekelezaji wa sheria nyingi nchini zikiwemo za ardhi, hali inayotokana na kuingiliwa na imani za kisiasa, jambo alilosema limeota mizizi katika maisha ya Wazanzibari.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi Faraji Shomari, alisema pamoja na kuwepo kesi 252 za migogoro ya ardhi mahakamani, ambazo kinadharia ni nyingi sana, alibainisha kuwepo kesi kadhaa nje ya mahakama hiyo, hali inayotowa sura ya ukubwa wa tatizo liliopo nchini.

Ameiomba Serikali kutoa msukumo katika kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria za ardhi zilizopo, akibainisha kuwepo kwa migongano katika baadhi ya sheria hizo, kati ya sheria moja na nyengine.

Aidha,Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nassor, alisema matumizi sahihi ya ardhi ni chanzo katika kukuza uchumi wa Taifa, hivyo akazitaka taasisi zinazohusika na masuala ya ardhi kufahamu mipango ya Nchi katika matumizi ya ardhi.

Salum alibainisha kuwa ni njia mojawapo katika kuepuka migogoro, hususan katika maeneo ya Uwekezaji.

Mapema, akiwasilisha mada juu “Sheria zinazosimamia matumizi ya Ardhi Zanzibar, Mrajis wa Ardhi, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Dkt Abdul-Nassir Hemed alisema Sheria za ardhi zilizopo nchini, ni miongoni mwa sheria bora Duniani, zikiwa na uwiano wa karibu na sheria za nchi nyingi, ikiwemo zile za ukanda wa Afika Mashariki.

Alitowa wito kwa Idara, Taasisi, Wizara na jamii kwa ujumla kuzitunza. Kuzisimamia vyema pamoja na kuziweka pamoja ili hatimae ziweze kusambazwa katika taasisi mbalimbali nchini.

Aidha, alisema ipo haja ya kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria ili ziweze kwenda sambamba na wakati uliopo kiuchumi, kijamii na kisiasa. 

Katika hatua nyengine, wadau walijadili ya hali ya Mchanga Zanzibar na Mwelekeo wake, na kuiomba Serikali kuwa makini iwapo itafikia hatua ya kufanya maamuzi ya kuagiza rasilimali ya mchanga nje ya nchi.
Walisema kuna umuhimu wa kuangalia usalama wa rasilimali itakayoingizwa, ilikuepuka uwezekano wa kuwa na wadudu au kemikali hatarishi.

Aidha,wameiomba Serikali kuishajiisha jamii juu ya matumizi mbadala ya mchanga, ili kuondokana na matumizi makubwa ya rasilimali hiyo wakati huu ikiwa imepungua.