UMOJA wa Mataifa (UN) umeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayosimamiwa na Mashirikia yake inatekelezwa kikamilifu na kupata mafanikio kwa azma ya kuwasaidia walengwa ambao ni wananchi wa Zanzibar.Mwakilishi Mkaazi na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) hapa Tanzania Alvaro Rodriguez alisema hayo leo wakati alipofika Ikulu kwa ajili ya kuaga na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Alieleza kuwa Mashirika yote ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayofanya kazi zake hapa Tanzania yanapongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein na kuahidi kuendelea kuunga mkono kwani wanafarajika na juhudi hizo.Alieleza kuwa Umoja wa Mataifa (UN) unapongeza sana juhudi hizo za Rais Dk. Shein na unaahidi kuendelea kushirikiana nae huku akieleza kuwa mashirika yote ya (UN) yana matumaini makubwa ya kuona matokeo endelevu yatakayotokana na juhudi hizo katika miaka ijayo.

Pia, kiongozi huyo alieleza azma ya Mashirika hayo ya UN katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, utawala bora, uimarishaji wa haki za binaadamu, uwezeshaji, mapambano ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto uhifadhi wa mazingira pamoja na mambo mengineyo.Mratibu huyo alieleza mafanikio yanayopatikana ambayo yamepewa kipaumbele katika utekelezaji wa ‘Programu ya pamoja ya Zanzibar ya mwaka 2018-2021’ iliyozinduliwa Agosti mwaka jana yakiwemo kupunguza vifo vya uzazi, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake kupitia zao la mwani pamoja na uratibu wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Mratibu huyo alieleza kuwa licha ya yeye kupangiwa majukumu mengine ya kikazi lakini anaamini kwamba kiongozi atakaye chukua nafasi yake ataendeleza uhusiano na mashirikiano mema yaliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na UN.

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Umoja huo chini ya Mratibu wake hapa Tanzania Alvaro Rodrigues ambaye amemaliza muda wake wa kazi hapa nchini kwa kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake wanampongeza Mratibu huyo kwa kuonesha moyo na juhudi kubwa za kuisaidia Zanzibar na kuiunga mkono katika miradi yake ya maendeleo wakati wa uongozi wote wa Rodrigues alipokuwepo nchini.

Aidha, Rais Dk. Shein alimtakia safari njema Mratibu huyo na kumtaka akaendelee kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa kama alivyofanya wakati akiwa hapa Tanzania.
Mapema Rais Dk. Shein, alifanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Bibi Jacqueline Mahol aliyefika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kuzungumza na Rais.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alilipongeza Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha huduma za jamii zinaimarika zikiwemo huduma za afya.Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Shirika la UNFPA limekuwa na uhusiano na ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu na tokea wakati huo limekuwa likifanya juhudi katika kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo.

Alieleza kuwa juhudi kubwa zimechukuliwa na mafanikio yanaonekana katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Washirika wa maendeleo likiwemo Shirika hilo la UNFPA.

Nae Mwakilishi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Bibi Jacqueline Mohan alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuimarisha miradi ya maendeleo pamoja na kuwapatia huduma wanawake na watoto.Mwakilishi huyo aliahidi kuwa Shirika lake litaendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kupambana na umasikini, kuwaletea maendeleo wananchi wake sambamba na kutekeleza Malengo na Mikakati yake iliyoiweka kwenye MKUZA III.

Katika maelezo yake, Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kuipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kupelekea lugha ya Kiswahili kupitishwa kwua lugha rasmi ya nne itakayotumika katika Jumuiya hiyo.Aidha, Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kutoka pole kwa ajali ya gari la mafuta iliyotokea hivi karibuni huko Morogoro na kusabisha vifo pamoja na majeruhi kadhaa.

Pia, Kiongozi huyo alipongeza juhudi za Zanzibar katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 sambamba na mafanikio makubwa yaliopatikana katika usajili wa vizazi kwa asilimi 71 na kueleza kwua (UNFPA), inajivunia mafanikio hayo yaliopatikana hapa Zanzibar.Hivyo, Shirika hilo limmeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kutoa misaada yake zaidi kwa kuendeleza miradi mbali mbali ambapo pia, Shirika hilo limeahidi kutoa msaada wa gari za mbili za kubebea wagonjwa (ambulances).

Pia, Shirika hilo limeeleza azma yake ya kuanzisha kampeni juu ya kukinga vifo vya watoto wachanga na wazazi na kuahidi kuzidisha mashirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya, elimu na nyenginezo.