MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuwatunza na kuwaenzi wazee ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii ili waishi maisha bora na yenye furaha.
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti huko katika ukumbi wa Afisi ya CCM Mkoa wa Mjini, Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati alipofanya mazungumzo na Wazee wa Wilaya ya Amani na Wilaya ya Mjini Kichama.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Sera ya Wazee na hivi sasa inaandaa Sheria ya kuwatunza wazee na kuwaenzi wazee hivyo, utaratibu wa kuwatunza wazee kwa kuwekwa taratibu na kanuni utafanyika na kwa wale wasiokuwa na vitambulisho vikiwemo vyeti vya kuzaliwa watajumuishwa.
Alieleza kuwa kuanzisha na kusimaimia uendeshaji wa programu maaluma ya huduma ya Pencheni Jamii ambayo imeagizwa na CCM katika Ilani yake ya Uchaguzi na alichokifanya yeye ni kutekeleza agizo hilo na kusema kuwa uwezo ukiruhusu Pencheni hiyo ataiongoza kabla ya kuondoka madarakani.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja kwa wazee kuwaeleza vijana juu ya heshima ya wazee na vipi wazee wanatakiwa kuenziwa na kutunzwa saambamba na kupema heshima yao kutokana na mambo makubwa waliyoyafanya.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea kupatikana uhuru wa Tanganyika na uhuru wa Zanzibar kupitia vyama vya ASP na TANU.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee ndio walioijenga Zanzibar na kuleta ukombozi na kuwakomboa wanyonge.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa na taarifa ya wazee hao waliyoisoma huku akieleza kuwa ahadi zote zilizoahidiwa na chama hicho zitatekelezwa hatua kwa hatua.
Alisisitiza haja ya kutumia busara ndani ya chama hicho sambamba na kuwatumia wazee katika kufanikisha masuala mbali mbali ndani ya chama hicho kwa maendeleo ya chama na maendeleo ya nchi kwa jumla.
Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ipo haja ya kupokea mawazo ya wazee sambamba na kuwaheshimu na kuwalinda wazee kwani kuna kila sababu ya kufanya hivyo hasa ikizingatiwa historia ya wazee wa nchi hii.
Rais Dk. Shein alipongeza kwa mapokezi makubwa aliyoyapata katika mikutano hiyo na kuzipongeza risala iliyotolewa ambayo imetoa pongezi kwawe na kwa Serikali anayoiongoza pamoja na wananchi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kutoa huduma za afya bure kwa wananchi wake na kutoweka kipaumbele kuanzisha Bima ya Afya kwani afya ni bure kwa Zanzibar.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Shein alieleza kuwa juhudi za makusudi zimechukuliwa katika kuhakikisha matibabu yanatolewa bure kwa wananchi hapa Zanzibar tokea uchunguzi wa maradhi hadi utoaji wa dawa.
Aliongeza kuwa huduma zote za afya hapa Zanzibar ni bure na amehakikisha Bajeti ya Wizara ya Afya inakuwa kubwa ili kukidhi mahitaji ya matibabu, hivyo Serikali haioni sababu ya kuweka Bima ya Afya kwani afya Zanzibar ni bure.
Alisema kuwa uchunguzi wa maradhi kupitia vipimo vya “MRI” “CT” Scan” “Exray” huduma za Patholojia zote zinatolewa bure kwa hapa Zanzibar.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia, imeweka elimu bure ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana katika sekta hiyo ikiwa ni misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Makamu mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza umuhimu wa wazee umo kwenye Katiba na Ilani ya CCM kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisisitiza haja ya kuijua na kuifahamu historia hatua ambayo alisema ndio iliyomsukuma kuanza kuzungumza na wazee kwani wao ndio waanzilishi wa Chama Cha ASP.
Aliongeza kuwa wakati huu uliopo ndio wakati mzuri wa kushikamana na kuwa kitu kimoja sambamba na kuongeza nguvu katika kukiimarisha na kukiendeleza Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisisitiza kuwa huu ni wakati wa kuwa kitu kimoja kati ya viongozi, wanachama na wazee wa CCM kufanya mambo yao kwa pamoja kati ya viongozi na wanaoongozwa tena bila ya kulaumiana.
Alieleza kuwa ushindi wa CCM katika chaguzi zake zote ni jambo ambalo halina mbadala kwani hilo ni agizo la Katiba ya Chama hicho kutokana na malengo iliyojiwekea.
Alisema kuwa chama hicho kinapendwa na wengi hivyo, kila lililopangwa na chama hicho ni vyema likatekelezwa.
Alisisitiza kuwa ushindi kwa CCM ni lazima ili Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 yaendelee kulindwa yadumishwe na yaendelezwe mbele.
Aidha, aliongeza kuwa ushindi kwa chama hicho ni muhimu kutokana na kuendelezwa na kudumishwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Alieleza kuwa tokea Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Zanzibar imebadilika sana na itaendelea kubadilika kwani yote hayo yanafanywa na CCM pamoja na viongozi wa Serikali na wananchi wake wakiwemo pia, nchi marafiki wanaoendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Sambamba na hayo, Makamo Mwenyekiti huyo alieleza kufurahishwa na mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Serikali iliyopo madarani na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hiyo ni kutokana na kuwa Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na inatekeleza Ilani ya chama hicho.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alisisitiza kuwa anachokitamka Rais Dk. Shein ndicho anachokitenda na yote aliyoyaahidi amekuwa akiyatekeleza kwa vitendo.
Naibu Mabodi alisema kuwa CCM itaendelea kuwatunza na kuwaenzi wazee kama ilivyoeleza Ilani ya Uchagauzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 huku akisisitiza kuwa CCM imewatambua wazee kwa kuweka Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote likiwemo Baraza la asili la Wazee wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui ambalo limeundwa siku ya pili baada ya kuundwa ASP.
Nao Wazee katika taarifa yao walimpongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Shein kwa kuwapatia wananchi huduma za kijamii yakiwemo maji safi na salama mjini na vijijini, afya na elimu bure sambamba na ujenzi wa majengo ya skuli za ghorofa kwa azma ya kuondosha changamoto zilizopo za elimu.
Walitoa ahsante na kumpongeza kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita ambao ulimpa kura nyingi zaidi ya asilimia 90 hatua ambayo imempelekea kutekeleza vyema na kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015- 2020.
Wazee hao wa CCM walimpongeza Makamo Mwenyekiti huyo kwa kuimarisha huduma za jamii na kueleza jinsi walivyofarajika kwa ujenzi wa mitaro ya maji jambo ambalo limeondosha mafuriko katika baadhi ya maeneo ya nyumba zao wanazoishi.
Kwa upande wa vituo vya afya, wazee hao walieleza kufarajika na juhudi kubwa zilizofanywa za ujenzi wa vituo vya afya katika Wilaya zao sambamba na kupatiwa vifaa tiba vya kisasa ambapo hatua hiyo imewawezesha wazee kupata huduma za afya karibu zaidi na kuweza kutibiwa maradhi yao madogo madogo bila ya kwenda Hospitali Kuu ya MnaziMmoja.
Walipongeza kwa utakarabari na ujenzi wa nyumba za wazee Sebleni kwa kuziezeka na kuzipaka rangi na kuziweka vifaa mbali mbali vipya huku huduma za wazee nazo zikiendelea kuimarishwa.
Walieleza kuwa maji safi na salama yamefikia asilimia 80, na wanamatumaini kuwa asilimia 20 zilizobakia zitafikiwa baada ya kumaliza mradi mkubwa unaotokana na mkopo wa India na matumaini yao wananchi wote watapata huduma hiyo katika maeneo ya Mji wa Zanzibar.
Walipongeza juhudi za ulinzi na usalama uliowekwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa kuwekwa CCTV kamera hatua ambayo imepelekeea kuimarika kwa amani na utulivu nchini sambamba na juhudi kubwa za ujenzi wa barabara za kisasa.
Walieleza furaha yao kwa kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar kwa kuongezeka kwa asilimia 7.2 kila mwaka na kupelekea wazee kupata Pencheni ya Jamii kwa kila mwezi jambo ambalo walisema fedha hizo zinawasadiia kuendesha maisha yao.
Wazee hao walimpongeza Dk. Shein kwa kusimamia Ilani kwa kuanzisha utaratibu huo wa kuwatunza wazee kwa kuwapatia elfu 20 kila mwezi.
Aidha, Wazee hao walimueleza Makamo Mwenyekiti huyo kuwa wataendelea kumuunga mkono pamoja na kuendelea kuiunga mkono CCM iendelee kushinda ili wazee pamoja na wananchi wote waendelee kuishi kwa amani, utulivu na mshikamano mkubwa.
Pia, wazee hao, walimpogeza Dk. Shein kwa kuwahudumia wananchi kwa kuwatekelezea sekta mbali mbali za maendeleo na kutumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. John Pombe Magufuli, kwa juhudi anazozichukua katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nao Wenyeviti wa CCM Wilaya ya Amani na Wilaya ya Mjini Kichama alimpongeza Rais Dk. Shein kwa uungwana wake kwani anachosema ndicho anachotenda kwani alisema kuwa ataibadilisha Zanzibar na tayari Zanzibar imebadilika kimaendeleo.